Serikali kupitia Wizara ya Afya
Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto imefanya ufunguzi wa mafunzo ya
mifumo ya afya iliyoboreshwa.Mafunzo haya yalianzia ngazi ya kitaifa,Mkoa na
sasa ni ngazi ya Wilaya na baada ya mafunzo haya taaluma hii itapelekwa ngazi
ya vituo vya afya.
Akifungua uzinduzi huo Katibu
Tawala wa Mkoa Bibi. Theresia Mmbando aliwapongeza Wizara ya Afya kwa kuandaa
mafunzo yenye tija katika sekta ya Afya. kwani mafunzo haya yatasaidia kupunguza
urasimu na kuboresha huduma za afya.
Mmbando alisema '' lengo mahususi
la mafunzo hayo kuwa ni uelewa mpana wa maana ya ugatuaji wa mipango ya Afya na
bajeti kwa utaratibu wa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma(DHFF)
yenye matarajio ya kupunguza urasimu na kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa
uandaaji wa mipango, bajeti na matumizi yanayolenga kuboresha huduma za Afya''.
Alifafanua zaidi mafunzo hayo
yamedhamiria kuwajengea uwezo watendaji wa ngazi ya mamlaka za Serikali za
mitaa. watendaji wa ngazi ya jamii, ambapo watendaji hao watakuwa wawekezaji
katika vituo vya kutolea huduma za Afya. Lengo kuu ni kutekeleza hatua za kuboresha
huduma za afya kupitia utaratibu wa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo ,
utekelezaji wa CHF iliyoboreshwa pamoja na mfumo wa wa kutumia MSHITIRI/JAZIA
(Prime Vendor-PVS).
Maboresho haya yatasaidia manunuzi ya dawa , vifaa, vifaa tiba na
vitendanishi pale vinapokosekana kutoka
Bohari kuu ya dawa(MSD).
Aliwashukuru pia wadau wa maendeleo kwa
kukubali kuendesha semina katika ngazi za Halmashauri ,Vituo vya kutolea huduma
pamoja na ngazi ya jamii.
Akizungumza na washiriki katika semina hiyo Dr. Mariam Ongara toka
Wizara ya Afya amesema kumekuwa na changamoto mbalimbali katika uendeshaji na
utoaji wa huduma katika maeneo mengi nchini hivyo kuifanya serikali kuchukua
hatua na kufanya mabadiliko ya kimfumo na kiuendeshaji ili kukabiliana na
changamoto hizo.
Vilevile alizungumzia mkutano wa
mwaka wa mapitio ya sekta ya Afya uliofanyika Dec 7,2016 iliamua kuanzisha
utaratibu wa kupeleka fedha moja kwa moja kwenye vituo vya kutolea huduma za
afya ili kuzipa nguvu zaidi kamati za usimamizi wa huduma za afya(HFGC) katika
kupanga na kusimamia huduma za afya katika ngazi ya jamii.
Utekelezaji wa mkakati huu
unalenga kugatua madaraka ya uendeshaji wa huduma za afya katika ngazi za vituo
ili kupunguza urasimu na kuboresha utoji wa huduma za afya. Katika kukabiliana
na changamoto hizo serikali kwa kushirikiana na wadau imeamua kutekeleza mfumo
wa CHF iliyoboreshwa ambao umekuwa ukitekelezwa katika mikoa mitatu ya Dodoma
Morogoro na Shinyanga ndani ya miaka mitano chini ya mradi wa Tuimarishe Afya
(HPSS)kwa mafanikio.
Mafunzo hayo yanafanyika kwa siku
tatu katika ukumbi wa Iddi Nyundo
Manispaa ya Temeke. watendaji zaidi ya 50 watapata mafunzo kutoka kwa wadau
wa mfuko wa Afya wa pamoja(Health Basket Fund), HPSS, PS3, Global Supply Chain
Program, Boresha Afya Deloitte, World Vision,EGPAF, Jhpiego, GIZ,AGPAHI na Pharmacies.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni