Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imekadiria
kukusanya kiasi cha sh. 251.7 kwa ajili ya matumizi mbalimbali kwa mwaka
2018/2019.
Akisoma bajeti hiyo katika kikao cha madiwani Mkurugenzi
wa Manispaa Ndg; Naseeb Mmbaga alisema kiasi hicho cha fedha kitapatikana
kutokana na vyanzo mbalimbali ikiwemo makusanyo ya ndani, ruzuku kutoka
serikali kuu na wahisani.
Alisema ndani ya kipindi hicho shilingi
219,076,455,243 zitatokana na ruzuku kutoka serikali kuu, sh.32,377,175,000 zitatokana na vyanzo vya
ndani na wahisani sh. 204,017,500.
Alisema tofauti na miaka iliyopita, bajeti ya
mwaka hu italenga zaidi miradi katika sekta ya afya,elimu ya sekondari na
msingi, miundombinu mbalimbali, mishahara na matumizi mengineyo.
''Lengo la bajeti ya mwaka huu kuona sekta hizi
muhimu nilizozitaja zinakuwa kwakasi katika kukabiliana na ongezeko la watu na
mahitaji yao ya kila siku'', alisema Mmbaga.
Akizungumza mara baada ya kupitishwa kwa bajeti
hiyo Mstahiki Meya wa Temeke, Abdallah Chaurembo, aliwataka watendaji na
madiwani kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kulipa kodi stahiki ili mipango
ya Halmashauri hiyo itekelezwe kwa wakati.
Alisema tayari elimu ya ukusanyaji kodi kwa
viongozi hao imetolewa na kilichobaki kufanya kazi kwa nguvu kuhakikisha kila
kata inakusanya mapato katika kiwango kinachotakiwa.
''Muda wa kusubiri ruzuku ya serikali kuu ili
mipango yetu ya maendeleo iweze kutekelezwa umekiwisha, lazima sisi wenyewe
tujitosheleze kifedha na hilo litafanikiwa kama sisi viongozi tutawajibika
kuwahimiza wananchi kulipa kodi'' alisema Chaurembo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni