Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mh. Felix
Lyaniva afanya uzinduzi utoaji wa chanjo ya kuzuia saratani ya mlango wa kizazi
katika shule ya sekondari Charambe ambapo zaidi ya watoto 40 wamechanjwa.
Chanjo hii itachanjwa kwa watoto
wenye umri wa miaka 14 kwa awamu ya kwanza, ambapo mpango wa kuwachanja mabinti
wote wa kuanzia umri wa 9-14 itafanyika kwa mwaka 2019.
Uzinduzi huo uliudhuriwa na wadau
mbalimbali akiwemo diwani wa kata ya Mianzini Mh:Abdallah Kipende,wataalam kutoka
Wizara ya Afya,wataalam wa Afya kutoka Manispaa,kamati ya ulinzi na usalama ya
Wilaya ya Temeke pamoja na viongozi wa dini.
Lyaniva alitoa shukrani zake kwa Rais
wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake za kuleta mabadiliko katika
sekta ya afya hususani afya za akina mama.Alisema '' serikali imetumia gharama
kubwa kutoa chanjo hii hivyo wazazi,walezi na jamii nzima tuhakikishe wasichana
wenye umri wa miaka 14 wanapata chanjo kwa awamu zote mbili bila kukosa''.
Lyaniva aliongeza chanjo hii
itapunguza wimbi la maambukizi ya saratani ya shingo ya kizazi katika taifa
letu hivyo wazazi msipuuze.
Akitoa somo kwa wanafunzi hao juu ya
saratani,mwakilishi kutoka Wizara ya afya Bi. Zuhra Mkwizu aliwataka wanafunzi wasiwe
na hofu kwani chanjo hiyo ni salama na haina madhara kabisa.
Alisisitiza kwamba Chanjo hii
imethibitishwa kitaifa na kimataifa na imethibitishwa na shirika la
afya Duniani (WHO).
"Chanjo hii ni salama na haina
madhara kabisa hivyo kuwataka baada ya miezi sita kurudia chanjo ya pili ili
kukamilisha dozi kamili"
Nao viongozi wa dini walipata wasaa
wa kuwausia watoto hao, namna ya kujilinda na kujichunga dhidi ya maambukizi ya
saratani ya mlango wa kizazi kwa kuepuka ngono zembe,kuacha tamaa.Huku wakitolea
mifano katika vitabu vitakatifu jinsi vinavyokataza kuacha anasa na dhambi.
Chanjo hii ilizinduliwa na Makamu wa
Rais kitaifa katika viwanja vya Mbaragala Rangi tatu na kwa sasa inaendelea
kutolewa katika maeneo mbalimbali nchini.
Katika Wilaya ya Temeke chanjo
hii itatolewa katika vituo 274,ambapo vituo 197 ni mashuleni na vituo 77 ni
katika vituo vya afya.Takribani wasichana 6,721 wanatarajiwa kupata chanjo ya
saratani ya shingo ya kizazi.Ambao itajumuisha idadi ya wale waliopo mashuleni
na nyumbani.